LOVE STORY

MUNGU mwenye nguvu na uweza wa ajabu ameendelea kuwa upande wangu. Ingawa ni mwenye dhambi na mara kwa mara nimemkosea, lakini hajauficha uso wake pale ninapomuita. Naam! Yeye ndiye mwenye enzi yote na tunapaswa kumuelekea yeye kwa kila hitaji.
Rafiki zangu, ukuu wa Mungu wetu ni wa ajabu sana. Hata katika uhusiano wako ukimuweka mbele yako, mambo ni rahisi kabisa. Nakukaribisha katika safu yetu ambayo hutupa maarifa mapya katika ulimwengu wa mapenzi.
Vijana wengi wamekuwa wakiwasiliana nami wakiuliza kuhusu uhalali wa kuoana katika imani za dini tofauti. Ni jambo lenye changamoto kubwa na limesabisha migogoro kwenye uhusiano wa vijana wengi.
Kutokana na uzito wake nikaona ni vyema nikaandika mada hii, lakini yenye mwendelezo zaidi kuhusu pia suala la kabila na mila.
SUALA LA DINI
Inasemwa sana kuwa, mapenzi hayachagui dini, kabila, rangi wala kitu kingine chochote cha kufananisha. Inaweza kuwa sawa, lakini kwa wakati mwingine siyo sawa hususan kwenye suala la imani ya dini.
Imani ni msingi wa maisha ya binadamu. Ni kile unachokiamini kimapokeo ambacho ni mwongozo sahihi wa maisha yako ya baadaye. Wakati mwingine mtu anaweza kubadili imani yake baada ya kuwa mtu mzima na huenda akapata mafundisho mapya ambayo yatamvutia na kuona ndiyo njia sahihi ya mwongozo wa safari yake hapa duniani.
Mwongozo huo ndiyo msingi. Kwa maneno mengine, kwa sababu kila dini ina msingi wa imani yake, ina miiko na taratibu zake, hutokea baadhi ya makatazo ya upande mmoja, upande wa pili ikawa halalisho.
Ni sahihi zaidi kuoana mkiwa katika imani moja ya dini, tena mnaoabudu katika tawi moja – ni nzuri zaidi. Hii itasaidia wote kuwa na mafundisho yanayofanana – hofu zinazofanana juu ya taratibu za maisha kwa utashi wa dini.
NI SAHIHI KUOANA DINI TOFAUTI?
Kisheria inakubalika. Pamoja na kukubalika huko, kama nilivyozungumza katika kipengele kilichopita ni rahisi kusababisha msuguano na kushindwa kupata utatuzi mzuri wa kiimani hasa kwa sababu imani ndiyo kimbilio na msingi wa kwanza katika maisha ya binadamu.
Wengi ni mashahidi juu ya ndoa za Kiserikali, hazina uhakika wa kudumu. Mnaoana leo, ukiona mwenzako huelewani naye baada ya wiki moja inaweza kubatilishwa na talaka kutolewa mara moja. Hii ni tofauti na zile za imani za dini, maana kabla ya kufikiria suala la talaka kuna njia za mazungumzo – mafundisho na ushauri wa kiimani zaidi.
Imani nyingi zinasisitiza sana suala la upendo na kusamehe, wakati kwenye sheria huangalia kwenye matatizo na matakwa ya ninyi mnaoamua kutengana.
NI SAHIHI KUBADILI DINI KWA SABABU YA NDOA?
Hili limekuwa likizua migogoro mara nyingi sana kwenye uhusiano wa vijana wengi. Wameanza uhusiano bila kugusia kabisa suala la dini. Baada ya kuzoeana na kila mmoja kuridhishwa na mwenzake, wanakuja kugundua kuna kikwazo cha dini. Hapa huanza kushawishiana mmoja wao (hasa msichana) kugeukia dini yake mwenzake ili waweze kufunga ndoa.

No comments:

Post a Comment